Wakampa. "Jini hili," akaendelea msichana, "limeninyakua usiku wa arusi yangu, likanifungia sandukuni kisha likalitia sanduku ndani ya kasha kubwa alifungalo kwa kufuli saba halafu hulizamisha katika lindi la bahari kuu ili eti nilindike! Atakapo, kama leo, hunitoa. Laiti angejua werevu na hila za wanawake!"
Shahriyar na Shahzaman kusikia vile wakastaajabu mno wakaambiana,"Kama kitendo kama hiki anaweza kutendewa jini mwenye nguvu kama huyu, hakika mikasa iliyotupata sisi haiwezi kulinganishwa na nusu ya vitendo vya msichana huyu!"
Basi bila kukawia wakarejea kwao mjini. Mara tu walipoingia katika kasri, Sultan Shahriyar akaamuru malkia wake na watumwa wake wakatwe vichwa.
Toka siku hiyo Sultan Shahriyar akawa hana imani tena na wanawake. Ikawa kila siku ni kumwoa mwanamwari mzuri na kumwua asubuhi ya pili. Aliendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka mitatu mpaka msiba mkuu ukaenea kote mjini na ukamkumba karibu kila aliyekuwa na binti mzuri mle mjini . Wengi wakauhama kwa kuwahofia mabinti zao.
Kazi hii ya kuhuzunisha alikuwa akifanyiwa Sultani na Waziri wake mpaka ikafika siku ambayo Waziri alishindwa kumpatia Sultani mwanamwari. Akarejea nyumbani kwake akiwa na wasiwasi na woga wa ghadhabu za Sultani.
Waziri alikuwa na binti zake wawili. Mkubwa aliitwa Shahrazad na mdogo aliitwa Dunyazad. Shahrazad alikuwa si mzuri wa sura tu, bali pia mwenye akili, busara na ujuzi wa kila elimu ya falme za kale. Alizidurusu na kuzihitimu vizuri mpaka akawa aalim wa mambo mengi. Siku ile akamwona baba yake mnyonge mwenye wasiwasi mwingi, akamwuliza lililokuwa likimkera.
Waziri akamweleza yale yaliyokuwa moyoni mwake. Shahrazad akasema, "Niache mimi niolewe na Sultani. Yatakuwa mawili: kufa au kuokoa maisha ya wasichana wenzangu waangamiao vibaya kila siku."
Ijapokuwa Waziri alifanya juu chini kumshawishi binti yake aache kusudio lake, hakufuzu. Shaharzad aling´ang´ania tu akubaliwe kuolewa na Sultani.Akaonya Waziri. Ndipo alipomsulimia mwanawe.
....THE END....
Home
Copyright © 2001 2002 Mombasa Web, Inc. All rights reserved..