Shahzaman akakubali. Wakatoka kwa siri wakasafiri kwa masiku mpaka siku moja wakafika pwani penye ufukwe mzuri mweupe wa bahari, ukingoni pake pameota majani mazuri yaliyokuwa yakipitiwa na chemchemi ya maji safi. Hapo wakashuka juu ya farasi zao, wakatawadha, wakasali sala ya adhuhuri. Baadaye wakawa wamebumzika kwenye kivuli cha mti mkubwa mmoja uliokuwa pale ukingoni wakila chakula chao cha mchana.
Mara bahari ikachafuka na kutoa mapovu na mawimbi yakaanza kupanda juu. Ghafla pale baharini pakazuka jabali refu jeusi lililokaribia mbingu. Lo! Kuona vile wale ndugu wawili wakapigwa na mshangao! Haraka wakapanda juu ya ule mti. Walipofika juu na kutazama baharini, wakaona kumbe lilikuwa si jabali bali ni jini lililobeba kasha kubwa kweli kweli kichwani pake! Likatoka mle baharini likaelekea pale mtini walipokuwa.
Baada ya kukaa chini, lile jini likafungua lile kasha, likatoa sanduku alilolifungua. Mle sandukuni mkatoka msichana mrembo mzuri kama nini! "Mwanamwali mzuri mtoto wa watu niliyekunyakua usiku wa arusi yako," likasema lile jini, "nataka kupumzika hapa kidogo." Mara, baada ya kutamka hayo, likalala pale kivulini na kukiegemeza kichwa chake juu ya mapaja ya yule msichana. Mara likachotwa na usingizi mzito likalala fofofo!
Katika kutazamatazama kwake huko na huko, yule msichana akanyanyua kichwa chake juu, kule mtini. Mara akawaona wale ndugu wawili. Kuwaona tu, akawaashiria washuke wasiogope. Lakini wale Sultani wakasitasita wakimsihi yule msichana azisalimishe roho zao.
Lakini msichana akasema, "kama hamtashuka, nitamwamsha jini na bila shaka yoyote atawaadhibu vikatili."
Waliposhuka, msichana akwaambia "Mkitaka usalaama wenu, ni lazima mfanye mapenzi nami sasa hivi tena hapa hapa!"
Shahriyar na Shahzaman wakakataa katakata lakini msichana akasisitiza kwa hasira, "kama hamtafanya nitakavyo, nitaliamsha jini!"
Basi wakawa hawana budi kuyatekeleza yale aliyoyataka yule binti. Baada ya kuwalazimisha wabaki naye kwa muda alioutaka, msichana akatoa kijaluba kibindoni mwake, akakifungua, akatoa pete tisini na nane zilizotungwa kwenye uzi wa hariri, kisha akasema huku akitabasamu kwa maringo na majivuno, "Mnaona! Wenye pete hizi wote wamelala nami wakati hili jini li hadhir limelala kama mfu! Na nyinyi ni lazima mnipe pete zenu sasa hivi!"
Endeleya!
Copyright © 2001 2002 Mombasa Web, Inc. All rights reserved..