Ndipo nikarejea kwenye msafara na nikaendelea na safari ya kuja huku, moyo wangu ukiwa umejaa huzuni na majonzi.
Aliposikia maneno haya kutoka kwa mdogo wake, Sultan Shahriyar akamsihi nduguye amweleze na ile sehemu iliyobaki, Shahzaman ikawa hana budi kumweleza kakiye yote aliyoyashuhudia pale bustanini.
Akipigwa na mshangao na kupandwa na ghadhabu lakini Sultan Shahriyar akasema, "Sitaamini hayo uyasemayo mpaka niyaone mwenyewe kwa macho yangu!"
"Kama ni hivyo," akapendekeza Sultan Shahzaman, "basi tangaza unakusudia kwenda tena mawindoni. Halafu urudi uje ujifiche nami hapa, nawe utayashuhudia niliyoya-shuhudia."
Basi Sultan Shahriyar akatangaza madhumuni yake ya kwenda tena kuwinda. Hapo kundi lake likatoka mjini huku limebeba matumizi ya Sultani kwa siku ile. Baada ya kubaki kidogo kambini kule mawindoni, Sultan Shahriyar akatoa amri kwa watumishi wake kuwa wasimruhusu yeyote kuingia hemani mwake. Halafu akajibadilisha, akarejea hadi kwake bila kuonekana na yeyote. Akamkuta mdogo wake anamsubiri. Wakajibanza na kuketi kwenye lile dirisha lililoelekea bustanini. Mara malkia na wajakazi wale wale wakatokea tena wakifuatwa nyuma na watumwa wale wale, wakayatenda yale yale waliyoyatenda siku ile!
Kuona vile Sultan Shahriyar akapigwa na bumbuazi na mshangao mkubwa sana. Akamgeukia mdogo wake akamwambia, "Ndugu yangu mpenzi, tuuache ufalme na tutokomee ulimwenguni tukatafute kama tutawapata waliokwisha kumbwa na mikasa kama hii."
Endeleya!
Copyright © 2001 2002 Mombasa Web, Inc. All rights reserved..