Site hosted by Angelfire.com: Build your free website today!

ALFU LELA U LELA

AU

USIKU ELFU NA MOJA

HAPO KALE paliondokea Sultani mmoja wa ki-Sassanid aliyekuwa na enzi kubwa iliyoenea toka Bara Hindi mpaka Uchina. Jeshi lake kubwa lenye nguvu, liliweza kuishindi na kuiteka kila nchi ya jirani na sifa za utawala wake zikaenea kila pembe ya dunia. Alipofariki, akawaacha wanawe wawili waliokuwa mashujaa na hodari wa kupanda farasi, hasa mkubwa aliyeitwa Shahriyar aliyerithi kiti cha enzi cha baba yake. Yeye alifuata nyayo za baba yake mpaka raia zake wote wakampenda. Mdogo wake aliyeitwa Shahzaman akawa Sultani wa nchi ya Samarkand.

Basi hawa wana Sultani wawili wakaendelea kutawala nchi zao kwa furaha na kwa haki kwa muda wa miaka ishirini mpaka siku moja Sultan Shahriyar akaingiwa na hamu kubwa ya kutaka kumwona mdogo wake. Basi akamwamuru Waziri wake aende Samarkand akamwalike.

Waziri akafunga safari. Baada ya safari ndefu ya siku nyingi katika jangwa, mbuga na nyika, akawasili katika mji mkuu wa Samarkand.

Bila kuchelewa akafikishwa mbele ya Sultan Shahzaman aliyefurahi sana kupokea salamu na ujumbe kutoka kwa kaka yake. Naye bila kuchelewa akatoa amri safari ya kumzuru kakiye itayarishwe. Akatanguliza msafara wa ngamia na farasi ulioshehenezwa vyakula na zawadi ukiongozwa na watumishi na wajakazi wake wa kumhudumia wakati wa safari yake ndefu. Kabla hajaondoka, akamchagua Waziri wake mkuu amshikilie madaraka yake mpaka atakaporudi. Matayarisho yalipokamilika, msafara ukang´oka.

Usiku Sultan Shahzaman akakumbuka amesahau zawadi muhimu aliyodhamiria kumpa kaka yake. Basi bila kuonekana na yeyote, akatoka hemani mwake akarejea kwenye kasri lake. Alipoingia ndani, lahaula!

Akamkuta mkewe amekumbatiwa kimapenzi na mtumwa wake mmoja! Kuona vile, akapigwa na bumbuazi na mshangao mkubwa. Hakuweza kuamini yale aliyokuwa akiyashuhudia pale penye sofa! Akafikiri: "Kitendo kama hiki kama kinaweza kutokea wakati sijafika mbali, iblisi huyu atafanya nini nitakapotoweka mbali?" Hapo akafuta upanga wake, akawaua wote wawili pale pale.

Endeleya!
    Copyright © 2001 2002 Mombasa Web, Inc. All rights reserved..