Usiku elfu na moja
HAPO ZAMANI ZA KALE paliondokea Sultani mmoja wa ki-Sassanid aliyekuwa na enzi
kubwa iliyoenea toka Bara Hindi mpaka Uchina. Jeshi lake kubwa lenye nguvu,
liliweza kuishindi na kuiteka kila nchi ya jirani na sifa za utawala wake zikaenea
kila pembe ya dunia. Alipofariki, akawaacha wanawe wawili waliokuwa mashujaa
na hodari wa kupanda farasi, hasa mkubwa aliyeitwa Shahriyar aliyerithi kiti cha
enzi cha baba yake. Yeye alifuata nyayo za baba yake mpaka raia zake wote
wakampenda. Mdogo wake aliyeitwa Shahzaman akawa Sultani wa nchi ya
Samarkand.
Basi hawa wana Sultani wawili wakaendelea kutawala nchi zao kwa furaha
na kwa haki kwa muda wa miaka ishirini mpaka siku moja Sultan Shahriyar
akaingiwa na hamu kubwa ya kutaka kumwona mdogo wake. Basi akamwamuru
Waziri wake aende Samarkand akamwalike.
Waziri akafunga safari. Baada ya safari ndefu ya siku nyingi katika jangwa,
mbuga na nyika, akawasili katika mji mkuu wa Samarkand.
Bila kuchelewa akafikishwa mbele ya Sultan Shahzaman aliyefurahi sana
kupokea salamu na ujumbe kutoka kwa kaka yake. Naye bila kuchelewa
akatoa amri safari ya kumzuru kakiye itayarishwe. Akatanguliza msafara wa
ngamia na farasi ulioshehenezwa vyakula na zawadi ukiongozwa na watumishi
na wajakazi wake wa kumhudumia wakati wa safari yake ndefu. Kabla hajaondoka,
akamchagua Waziri wake mkuu amshikilie madaraka yake mpaka atakaporudi.
Matayarisho yalipokamilika, msafara ukang´oka.
Click on the following links to see more on msa.islovely.com